Yeremia 35:12-19 - 20-06-2026

Date
Reading
Yeremia 35:12-19

Jumamosi asubuhi tarehe 20.06.2026;

Yeremia 35:12-19
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,

13 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema Bwana.

14 Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi.

15 Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza.

16 Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi;

17 kwa sababu hiyo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize; nimewaita, wala hawakuniitikia.

18 Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote, na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru;

19 basi, kwa sababu hiyo, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.

Yesu ni mlango wa kuingia mbinguni;
Leo tunasoma Yeremia akitumwa kupeleka ujumbe kwa Yuda na Yerusalemu yote, kwamba kwa nini walikuwa wamekataa kupokea mafundisho ya Bwana. Hawakusikiliza neno la Mungu, pamoja na kwamba walipelekewa walimu na manabii wa kutosha. Yeremia anatumwa kuwaambia kwamba haikuwa sawa kwao kutomsikiliza Mungu kwa njia ya watumishi wake.
Yeremia anasema Bwana ataleta mabaya juu yao wasipomsikiliza. Wakitii atawabariki, nao watasimama mbele za Mungu hata milele. Ujumbe wa leo asubuhi kwetu ni kumsikiliza na kumtii Bwana kwa njia ya neno lake. Tusome neno la Mungu, tuhudhurie ibada, na kusanyiko lolote linalofaa kwa taratibu za Kanisa. Huko tunafundishwa neno la Mungu, tukikumbushwa kumshika Kristo aliye mlango wa kuingia mbinguni. Amina
Siku njema

Heri Buberwa